Benin kuchangia wanajeshi 2,000 kwa kikosi cha Kenya nchini Haiti

 

Benin imejitolea kuchangia wanajeshi 2,000 kwa kikosi cha usalama cha kimataifa kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa kupambana na ghasia za magenge nchini Haiti.

Tangazo hilo lilitolewa Jumatatu wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Georgetown, Guyana, na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield.

Bi Thomas-Greenfield alisema alikuwa amejadiliana na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry na washirika wengine kuhusu umuhimu wa ''kupeleka haraka" kikosi hicho.

"Dhamira hii ni muhimu katika kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti kurejesha amani na usalama, kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, na kupunguza mzozo wa kibinadamu," Bi Thomas-Greenfield alisema.

Maafisa hao walitarajiwa kwenda Haiti mwezi huu, lakini mpango huo ulicheleweshwa baada ya kuzuiwa na mahakama ya Kenya mwezi Januari.

Mahakama ilisema kuwa serikali haina mamlaka ya kutuma maafisa wa polisi nje ya Kenya.

Lakini muda mfupi baada ya uamuzi huo, Rais wa Kenya William Ruto alihakikisha kuwa Kenya bado itawapeleka maafisa hao wa polisi baada ya kukamilisha makaratasi ya kukidhi matakwa ya mahakama.

Ghasia za magenge zimezidi kuwa mbaya zaidi nchini Haiti.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mwezi uliopita, magenge ya Haiti yaliua watu 8,400 mwaka jana, ongezeko la 122% kutoka 2022.

 

About MWESI MEDIA

Asante Mfuatiliaji wa Mwesi Media Ukiwa na Maoni au Jambo lolote Kuhusu Taarifa Zetu Tafadhali Wasiliana nasi 0757 056 462 Asante na Endelea Kubaki nasi.

0 Comments:

Post a Comment