SINGIDA
Timu ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, ikiongozwa na Mstahiki Meya, Mhe. Yagi Kiaratu, pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa, Bi. Joanfaith Kataraia, leo Januari 29, 2025 wameitembelea Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Viongozi hao, wakiwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, wamejikita katika kujifunza mbinu bora za ukusanyaji wa mapato, usafi wa mazingira, na ukusanyaji wa ada ya taka katika Manispaa.
Pia wanatarajia kujifunza juu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na mikakati mingine inayohusiana na ujenzi wa Manispaa bora.
Mhe. Kiaratu alisema kuwa ziara hiyo inalenga kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa Manispaa ya Kinondoni, ambayo inafanya vizuri katika masuala ya ukusanyaji mapato na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Aliongeza kuwa mafanikio ya Manispaa ya Kinondoni katika kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo ni mfano mzuri wa kile kinachoweza kufikiwa endapo kutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi.
Viongozi hao wamepata mafunzo ya kina kuhusu njia bora za ukusanyaji mapato, jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa Halmashauri yoyote, kwani mapato ndio yanayoifanya Manispaa kuwa na uwezo wa kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Manispaa ya Singida kuhakikisha kuwa inakua kiuchumi na kijamii kwa kuboresha mifumo ya kiutawala na usimamizi wa raslimali.
0 Comments:
Post a Comment