Na Glory Izack
Afisa habari mkoa wa Singida
Maafisa elimu nchini wametakiwa kusimamia suala la wanafunzi kupata chakula shuleni ili waweze kupata ufanisi katika masomo yao na kuondoa ukondefu kwa watoto wao.
Naibu katibu mkuu ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Elimu Atupele Mwambene ametoa wito huo leo (Januari 27,2025) wakati akizungumza na Maafisa Elimu kutoka mikoa yote ya Tanzania bara katika kikao kazi cha tathimini utekelezaji wa shughuli za Elimu kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2024.
Aidha katika hatua nyingine amewataka viongozi wote kusimamia weledi na kusuluhisha matatizo wakiwa kazini.
Akizungumzia katika kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga amewakaribisha Maafisa hao Mkoani Singida, kwenda kuwaandaa wanafunzi ili ufaulu wao uendane na uhalisia uliopo(upatikanaji wa miundombinu bora)kwa kuhakikisha wanapata chakula chenye virutubisho bora ili kuongeza afya ya mwili na ufaulu wao katika masomo.
Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya Maafisa Elimu wanaoshiriki kikao hicho wanasema vikao hivyo vinaendelea kuleta tija katika utendaji wao wa kazi na kuleta matokeo chanya kwenye sekta hiyo.
Kikao hicho cha tathimini utekelezaji wa shughuli za elimu kinawakutanisha maafisa elimu mikoa na wilaya zote nchini na kinatarajiwa kufanyika kwa siku tatu huku kauli mbiu ikiwa ni "Utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi ni msingi wa Elimu bora.
Katibu tawala Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga.
0 Comments:
Post a Comment