Kutokana na
changamoto za kimazingira, kiuchumi na kijamii, watu wengi wamejikuta wakikosa
furaha. Ni wazi kuwa kukosa furaha kuna madhara makubwa kwenye afya ya mwili, akili
na hata katika utendaji wako wa kazi.
Watu
wengi hutamani kuwa na furaha lakini bado hawapati furaha; wengi hudhani kuwa
na vitu kama vile pesa ndiyo chanzo cha furaha, lakini mambo hayawi kama
walivyotarajia pindi wapatapo vitu hivyo.
Je
unahitaji kuwa na furaha ili uboreshe afya na ufanisi wa utendaji kazi wako?
Karibu nikushirikishe njia 10 za kukufanya kuwa na furaha.
1. Samehe
Watu
wengi hukosa furaha kutokana na kubeba uchungu na maumivu yaliyotokana na watu
waliowakosea. Ikiwa unataka kuwa na furaha ni muhimu kumsamehe aliyekukosea
hata kama hajaomba msamaha.
Kumsamehe
aliyekukosea kuna manufaa kwako zaidi kuliko kwa yule aliyekukosea. Mara nyingi
aliyekosea huendelea na maisha yake ya kawaida huku aliyekosewa akizidi kuumia.
2. Fanya unachokipenda
“Mafanikio
siyo ufunguo wa furaha. Furaha ni ufunguo wa mafanikio. Kama unapenda
unachokifanya, utafanikiwa.”
Albert Schweitzer
Moja kati
ya siri kubwa ya kufanikiwa na kuwa na furaha katika kile unachokifanya, ni kwa
kupenda kile unachokifanya. Unapopenda kile unachokifanya, utakuwa na amani na
furaha mara ukutanapo na changamoto au vikwazo.
3. Kuwa na shukrani
Mara
nyingi tunatazama mambo mengi kiasi cha kushindwa kuwa na shukurani kwa yale
tuliyonayo. Ni rahisi kuona kuwa mambo kama vile afya, marafiki, usalama,
malazi n.k. ni mambo madogo ambayo hatupaswi kushukuru kwa ajili yake.
Kwa
hakika wapo watu wanaotafuta mambo hayo lakini hawayapati. Hivyo ili kupata
furaha ni muhimu kutambua na kushukuru kwa yale machache tuliyonayo.
4. Saidia wengine
Kumsaidia
mtu mwingine siyo kumpa pesa au vitu; hata kumpa mtu ushauri au kumtia moyo
kunaweza kuwa na maana kubwa kwa mtu huyo.
Unapomsaidia
mtu mwingine unajisikia kuwa na thamani na furaha kwani umeweza kufanya kitu
chenye manufaa kwenye maisha ya mtu mwingine.
Nakumbuka
niliwahi kumshauri mtu mmoja aliyekuwa amekata tamaa kutokana na kukosa pesa;
baada ya muda kupita nikakutana naye, akashukuru sana kwa ushauri wangu.
Alinieleza kuwa kama siyo yale maneno niliyomweleza angekuwa ameshajiua. Ni
wazi kuwa nilijihisi mwenye furaha na amani kutokana na kuweza kumsaidia mtu
mwingine.
5. Shirikisha wengine
Inawezekana
jambo linalokukosesha furaha kuna mtu mwingine anafahamu utatuzi wake. Hivyo
kwa njia ya kumshirikisha mwingine utapata ushauri au hata utatuzi wa tatizo
lako. Jambo la kuzingatia ni kuhakikisha unamshirikisha mtu sahihi.
6. Ondoa mawazo hasi
“Akili ni
kila kitu. Unavyofikiri ndivyo unavyokuwa.”
Buddha
Mawazo
gani uliyonayo kwenye fikra zako? Je unawaza tu huwezi au kushindwa? Mawazo
hasi au ya kushindwa ni chanzo kikuu cha kukukosesha furaha.
Amini
unaweza hatakama unaona giza; leo ni giza, kesho ni mvua lakini keshokutwa jua
litawaka.
Usikate
tamaa, ondoa mawazo mabaya yanayokufanya ukose furaha na mani sasa.
7. Usitafute ukamilifu
Mara
nyingi watu hukosa furaha kwa sababu wanatafuta ukamilifu. Kwa hakika hakuna
binadamu aliyekamilika; wote tuna madhaifu na mapungufu ya aina mbalimbali.
Badala ya
kuyatafakari madhaifu yako na kuruhusu yakukoseshe furaha; yakubali na
ukabiliane nayo kwa namna bora zaidi.
8. Kaa na watu sahihi
Je umekaa
katikati ya watu wanaokulaumu, kukudharau au kukubeza kila wakati? Au pengine
umekaa katikati ya watu walioshindwa wanaolaumu na kulalamikia kila kitu?
Watu wa
aina hii wanakusababisha ukose furaha. Hakikisha unakaa katikati ya watu
wanaokutia moyo na kukuthamini. Epuka watu walioshindwa ambao kazi yao kubwa ni
kulalamika na kulaumu kila kitu.
9. Ishi maisha yako
“Muda
wako ni mdogo, usiupoteze kuishi maisha ya mtu mwingine.”
Steven Jobs
Watu
wengi hukosa furaha kutokana na kuishi maisha ya watu wengine. Jikubali ulivyo,
usitake kuwa kama mtu mwingine kwani hutoweza na utaishia kukosa furaha. Tambua
wewe ni wa pekee na tembea katika upekee wako huo.
10. Jiburudishe
Je unajua
kuimba? Je unapenda michezo au kusikiliza mziki? Kama jibu ni ndiyo, basi hii
ni njia mojawapo amabayo inaweza kukupa furaha.
Ikiwa
umekosa furaha, unaweza kuimba, kusikiliza mziki au hata kushiriki kwenye
mchezo unaoupenda
Hitimisho
Naamini
sasa baada ya kusoma makala hii juu ya njia za kupata furaha, hutokosa tena
furaha maishani mwako.
Usiruhusu
vitu vya dunia hii vinavyopita vikunyime amani na furaha; maisha ni bora zaidi
kuliko vitu.
0 Comments:
Post a Comment