IGUGUNO YAPATA KITUO CHA AFYA


 SINGIDA 

Wananchi wa Kata ya Iguguno, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wamechangia Sh. milioni 12.96 kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Afya Iguguno, ambacho kimegharimu jumla ya Sh. milioni 262.96 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kituo hicho uliofanywa na Mwenge wa Uhuru, Mbunge wa Iramba Mashariki, Jesca Kishoa, amesema kituo hicho kitakuwa suluhisho la changamoto ya wananchi wa Iguguno waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Singida Mjini kupata huduma za matibabu. 

Kishoa ameishukuru serikali kwa kutoa Sh. milioni 250 zilizowezesha kukamilika kwa mradi huo.

Akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali ya kuboresha huduma za afya na kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Mkalama.

Pia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang'onda, amesema ujenzi wa kituo hicho ni faraja kwa wananchi wa Iguguno na kata jirani, huku akiwataka kuendelea kudumisha amani na utulivu ili serikali iendelee kutekeleza miradi mingine ya maendeleo katika eneo hilo.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Iguguno, Jackson Mirashi, amesema kituo hicho kitaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kata ya Iguguno na maeneo ya jirani ikiwemo Kikhonda, Kinyangiri na Tumuli, pamoja na Msisi (Halmashauri ya Singida), Mbelekese (Kata ya Kisuluda) na Maluga zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.

Amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 61,251

Aidha, mradi huo umezalisha ajira kwa wananchi 36 wa Kata ya Iguguno, wakiwemo wanaume 27 na wanawake tisa.






About MWESI MEDIA

Asante Mfuatiliaji wa Mwesi Media Ukiwa na Maoni au Jambo lolote Kuhusu Taarifa Zetu Tafadhali Wasiliana nasi 0757 056 462 Asante na Endelea Kubaki nasi.

0 Comments:

Post a Comment